Utajiri: Suti Zamtajirisha Bilionea Delano


Ukweli ni kwamba, utajiri si bahati. Ni matokeo ya juhudi zako. Ni matokeo ya yale unayoyafanya katika kipindi chote.
Huwezi kusema kwamba umeandikiwa bahati, hivyo ukae chumbani, ujifungie na kusema kuwa, utajiri utakuja tu kwa kuwa umeandikiwa. Bilionea Said Salim Bakhresa, asingeweza kuwa tajiri kama tu angesema kwamba, anakubaliana na hali aliyokuwa nayo kipindi hicho na kukaa tu kwa kuamini ungemfuata.
Nigeria ni moja ya nchi zenye mabilionea wengi hapa Afrika.
Nchi hiyo iliyopo Magharibi mwa Afrika imekuwa ikiongoza kwa miaka kadhaa kuwa na mabilionea, vijana wachapakazi ambao wamepambana kutoka kwenye umaskini na mwisho kuwa mabilionea wakubwa.
Miongoni mwa vijana hao ni Sijibomi Ogundele, Igho Sanomi na wengine wengi.
Mbali na mabilionea hao, leo tunakwenda kumtambua bilionea mwingine kijana ambaye anatikisa kwa kipindi kirefu nchini Nigeria. Ni jamaa anayeitwa Ladi Delano, bilionea mwenye umri wa miaka 37 tu
UTAJIR WAKE
Jamaa ana utajiri mkubwa wa dola bilioni moja hivyo ana jambo la kujifunza kutoka kwake.
 MASKINI KAMA WENGINE
Delano anasema kwamba hakuzaliwa kwenye familia ya kitajiri ila anashukuru kwa sababu baba yake alikuwa mfanyabiashara mdogo kwa
hiyo kila siku alikuwa akimwambia kuhusu kufanikiwa.
Hakuwa akipenda biashara, lengo lake kubwa lilikuwa ni kuwa mwanasheria. Lakini baada ya baba yake kumwambia mengi kuhusu biashara na kwamba angefanikiwa zaidi ya kuwa mwanasheria, alibadili mawazo yake na kuwa mfanyabiashara.
Anaendelea Kusema kwamba katika maisha aliyokuwa akiishi, alitamani sana kumiliki laptop (kompyuta mpakato) lakini alishindwa kwani kumwambia baba yake amnunulie ilihali yeye mwenyewe alikuwa akipambana na umaskini, lilikuwa jambo gumu.
AANZA KUUZA SUTI
Delano anasema alianza kufanya biashara kwa kuuza suti nchini Nigeria. Ilikuwa biashara nzuri na ilimlipa sana kwani suti zake nyingi aliwauzia matajiri ambao walimlipa fedha nzuri hivyo kuzikusanya, akaziongezea na alizopewa na baba yake kisha akaenda zake nchini China.
 BIASHARA YA POMBE CHINA
Delano anasema kuna kipindi alimuomba baba yake kwenda China kwani aliamini huko kulikuwa na fedha nyingi na kwa sababu baba yake alitaka kufanikiwa, akamtafutia fedha na kwenda huko. Akiwa China alijitafutia michongo ambayo hakuweka wazi na kuanza kuuza pombe za rejareja nchini humo.
 AANZISHA KAMPUNI
Baada ya kufanikiwa, Delano aliamua kuanzisha kampuni yake nchini China. Hiyo ilikuwa mwaka 2004, kampuni hiyo iliitwa Salidarnosc Asia, kampuni ambayo inatengeneza pombe iitwayo Solid XS.
Pombe hiyo ilimpa mafanikio makubwa kwani ilikuwa ikiuzwa katika miji ishirini na kwa mwaka alikuwa akikusanya dola milioni 20 (zaidi ya shilingi bilioni 40) kama faida, japokuwa baadaye aliamua kuiuza kwa dola milioni 15 (zaidi ya shilingi bilioni 30).
Delano anasema kwamba baada ya kurudi nchini Nigeria, aliumizwa na hali aliyoikuta kwani asilimia 43 ya vijana walikuwa maskini hivyo aliahidi kuwasaidia kwa kuanzisha kampuni zake na kuwaajiri.
Mwaka 2005 alianzisha Kampuni ya Bakrie Delano ambayo inahusika na madini, gesi, mafuta na kilimo. Mwaka 2012, Delano alitajwa kwenye orodha ya Forbes ya mabilionea wa kufuatiliwa zaidi.
 TUNAJIFUNZA NINI?
Delano anapohojiwa na vyombo vya habari, anasema kilichomfanya kuwa bilionea si bahati bali ni kufanya kazi kwa bidii huku akiendelea kusema kwamba hakuna binadamu asiyefanya makosa.
Kama wewe ukimuoneshea mtu aliyefanikiwa bila kufanya makosa, yeye atakuoneshea mtu asiyefanya makosa na bado hajafanikiwa. Hivyo tupambane na tusiogope kukosea kwenye biashara.

MPENDWA MSOMAJI WETU TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

Latest


EmoticonEmoticon